Na Sabina Chrispine Nabigambo
Wananchi wa Afrika Kusini leo Jumapili wanaungana kwa pamoja makanisani, misikitini, hekaluni na kwenye masinagogi , kufanya ibada ya kumkumbuka rais wa kwanza mweusi wa taifa hilo Nelson Mandela ambaye ujumbe wake wa amani na maridhiano enzi za uhai wake uliondoa matabaka ya dini na rangi.
Siku hii ya kitaifa iliyotengwa maalumu kwa ajili ya sala kumkumbuka Mandela ni mwanzo rasmi wa kuelekea mazishi ya kitaifa kwa kiongozi huyo muhimu aliyeasisi taifa jipya la Afrika kusini lenye watu wa jamii mchanganyiko,baada ya utawala wa kibaguzi ambao alisaidia kuuondosha.
Rais wa Marekani Barack Obama na mkewe Michelle Obama watahudhuria ibada ya kumbukumbu jijini Johannesburg siku ya Jumanne,akiwa ni miongoni mwa viongozi wengi wa dunia wanaotarajiwa kufika nchini Afrika Kusini kutoa heshima zao za mwisho kwa shujaa huyo wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi.
Rais Jacob Zuma amesisitiza kuwa ibada za leo Jumapili zinapaswa kufanyika huku zikiweka kando huzuni kusherehekea kwa uwazi urithi wa Mandela ambaye alifariki dunia siku ya Alhamisi akiwa na umri wa miaka 95,baada ya kuugua kwa muda mrefu.Zuma amesema kuwa pamoja na kuomboleza, wananchi waimbe kwa sauti za juu, wacheze na kufanya chochote watakacho, kusherehekea maisha ya mwanamapinduzi na baba wa taifa lao.Siku ya Jumanne watu wapatao elfu themanini ikiwa ni pamoja na Rais Obama wanatarajiwa kuhudhuria ibada maalumu ya kumkumbuka Mandela,kwenye uwanja wa michezo wa Soweto, uwanja ambao ulitumika katika mashindano ya kombe la dunia mwaka 2010.
Source: kiswahili.rfi.fr/dunia