Na Lucy Mgina
KISASI! Kisasi! Kisasi! Timu ya wabunge mashabiki wa Simba wameongeza nyota wanne kwenye kikosi chao ambacho kitavaana na kile cha wabunge wa Yanga ili kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwenye mchezo wa Tamasha la Usiku wa Matumaini, Jumapili ijayo.
Hii ni mechi kali ambayo itapigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na mashabiki wanaisubiri kwa hamu kubwa kuona ni timu gani inaweza kuibuka na ushindi.
Hiki ni kama kisasi, kwani Yanga awali waliwaongeza wachezaji wanne, Athumani Iddi ‘Chuji’, Kelvin Yondani, Mrisho Ngassa na Ally Mustapha ‘Barthez’.
Nyota wa Simba walioongezwa ni beki wa pembeni Said Nassor ‘Chollo’, Shomari Kapombe, kiungo mshambuliaji Amri Kiemba na winga mwenye kasi, Ramadhan Singano ‘Messi’. NA GLOBAL PUBLISHER
Akizungumza na Championi Jumatano, beki wa wabunge wa Simba, Chollo, alisema hawatishwi na Yanga ambayo nayo imeongeza vijana na watahakikisha wanalipa mabao 2-0 waliyofungwa kwenye ligi ili kuwafuta machozi mashabiki wao.
Alisema wana imani na kikosi chao ambacho kipo fiti na hakitishwi na maneno ambayo wapinzani wao Yanga wameyazungumza na kwamba wao ni watu wa vitendo tu, hivyo siku hiyo ni lazima waondoke na kombe lao jipya.
Kwa upande wa Messi, alisema wana machungu ya kupoteza mechi ya ligi kuu lakini wanashukuru kwa kuwa mchezo huo utakuwa kama wa marudiano, hivyo Yanga lazima wapigwe.
Alisema kawaida yake ni mbio tu, hivyo Yondani na mabeki wenzake wa Yanga watawafanya nyanya siku hiyo kwa kuhakikisha wanawafunga mabao ya mapema zaidi na wanawaomba mashabiki wao kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Taifa, Jumapili ili kuwaunga mkono.
“Mashabiki wa Simba wasiwe na hofu na maneno ya Yanga, tumejiandaa vyema kuhakikisha tunawachapa ili tuondoke na kombe letu, Yanga kitu gani bwana?
“Naomba mwamuzi anilinde siku hiyo kwani nitawaaibisha mabeki wao, ohoo! Wengi wanajua staili yangu ya uchezaji ni kasi mwanzo mwisho, ni vyema mashabiki wakaja kutuunga mkono ili tuwamalize mapema,” alisema Messi.
Kwa upande wa Yanga, kiungo Athuman Idd ‘Chuji’, alisema mwaka huu ni wao kutamba kisoka na kila anayekatisha mbele yao lazima aache pointi tatu, hivyo Simba wajiandae kwa kichapo ili wakasimulie kwao.
“Kelele za nini? Mashabiki waje uwanjani waone aibu tutakayowapa hao Simba, tunataka kumalizana nao mapema ili wakalale, watuache wakubwa zao tukishangilia kwa kutwaa kombe la pili baada ya lile la ligi kuu,” alisema Chuji.
Aidha, mratibu wa tamasha hilo, Abdallah Mrisho ‘Abby Cool’, amesema ulinzi utakuwepo kwa asilimia 100 na mashabiki wanaruhusiwa kuhudhuria na familia zao kupata burudani.
Alisema kutakuwa na jeshi la polisi ambalo litasimama kidete kuhakikisha mashabiki watakaojitokeza siku hiyo wanakuwa katika mikono salama, pia farasi na mbwa watakuwepo kuweka ulinzi.
Aliongeza kwamba maninja zaidi ya 60 watakuwepo uwanjani hapo mwanzo wa shoo hadi mwisho na mabaunsa ambao watakuwa tayari kuhakikisha usalama ni wa kutosha kabisa.
“Napenda kuwahakikishia mashabiki katika suala la ulinzi kuwa utakuwepo kwa asilimia 100, tutakuwa na farasi, mbwa na maninja ili kuhakikisha watu wote watakaojitokeza hapa, wanaondoka katika mikono salama,” alisema Abby Cool.
Burudani nyingine zitakazokuwepo siku hiyo ni wakali wa muziki, Nasibu Abdul ‘Diamond’ na Prezzo, ambao watashindana katika jukwaa moja ili kutafuta nani mkali zaidi.
Bendi za Msondo Ngoma, Mlimani Park ‘Sikinde’ na Jahazi zitawaburudisha mashabiki wao. Vilevile, burudani nyingine itatoka kwa wakali wa Temeke, Wanaume Family na Halisi, wataokata mapanga Taifa kwa staili zao za kuvutia.
Soka la kukata na shoka kati ya Bongo Movie na Bongo Fleva litahakikisha linawapa raha mashabiki wa wasanii watakaoingia uwanjani siku hiyo.
Pia kutakuwa na ndonga za ‘kukata na mundu’ kutoka kwa mabondia wa Kenya na Tanzania ambapo Mkenya, Patrick Amote atachapana na Thomas Mashali, wakati Shadrack Muchanje wa Kenya ataonyeshana ubavu na Mtanzania Francis Miyeyusho.
Ngumi za utangulizi zitapigwa na msanii Vincent Kigosi dhidi ya Mbunge Zitto Kabwe, msanii Aunt Ezekiel atapambana na mbunge Ester Bulaya, wakati mwanadada Jacqueline Wolper atavaana na mbunge, Halima Mdee.