Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF) kwa kushirikiana na PSI Tanzania na Shirika linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA) wametoa mafunzo ya afya kupitia jukwaa maalumu la wanawake (Women Panorama) katika tamasha hilo.
ZIFF kwa kushirikiana na PSI na UNFPA waliamua kutumia jukwaa la wanawake liwe maalumu kwa kutoa elimu ya uzazi wa mpango kwa vijiji saba kutokana na ukweli kwamba Tanzania ni mojawapo ya nchi ambazo zina viwango vya juu vya vifo vya wanawake vitokanavyo na matatizo ya uzazi.
Uzazi wa mpango hupunguza vifo vya uzazi kwa theluthi 3. Kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa mwaka 2010 na Taasisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) karibu wanawake 20 hufariki kila siku kutokana na matatizo hayo.
Wakiwa katika kijiji cha Jambiani Kibigija katika Kata ya Wilaya ya Kusini Mkoa wa Unguja Kusini Bi Fatma Ally Khatibu kutoka kitengo cha Elimu ya Afya Wizara ya Afya alitoa elimu ya uzazi wa mpango kiwemo njia mbalimbali za uzazi wa mpango pamoja na faida zake kiafya na kiuchumi.
Wakitoa maoni yao katika kijiji hicho wanawake wa Jambiani walisema wanaelewa umuhimu wa kupanga uzazi ila wanaume wao ndio wamekuwa vikwazo katika kupata elimu hyo.
“Tunaomba mafunzo haya pia yashirikishe wanaume maana wanaume wengi wamekuwa wakiwazuia wake zao kutumia uzazi wa mpango maana hawajui ukweli kuhusu uzazi wa mpango matokeo yake wanawake wengi wamekuwa wakifanya maamuzi bila kuwashirikisha wanaume”, alisema Amina Salim Ally.
Aliongeza kuwa baadhi ya wanaume wamediriki kwenda kufanya fujo vituo vya afya ili waoneshwe orodha ya wanawake wanaopata huduma hiyo na wakibaini wake zao ni mojawapo wakirudi nyumbani huwapiga sana wake zao.
Mbali na kuomba warsha kama hyo kwa wanaume, wanawake hao pia waliwaaomba wataalamu kutembelea kwenye mashule na kutoa elimu ya afya na haswa suala la kuepuka ngono ili kuepuka mimba katika umri mdogo.
“Watoto wa siku hizi wamekuwa watukutu tunajaribu kuongea nao ila bado wapata mimba halafu wanaenda vichochoroni kutoa hivyo kama elimu itakuwepo shuleni na wakirudi nyumbani tukiwaambia itawasaidia kuepuka ngono” alisema Taile Mzee.
Baada ya warsha hiyo ilokuwa maalumu kwa wanawake, wanakijiji wote wa Jambiani wakati wa jion walipata fursa ya kuangalia filamu mbalimbali zenye kutoa elimu ya afya.
Filamu hizo zilizooneshwa kwenye jukwaa la ZIFF, wanakijiji walipata kujifunza jinsi ya kutibu maji ya kunywa yawe safi na salama na jinsi ya kuyatunza. Na pia walipata kujifunza umuhimu wa kunawa mikoni mara baada ya kutoka chooni.
Mbali na hayo filamu ilooneshwa pia ilikuwa na mafunzo ya umuhimu wa kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama peke yake mpaka anapotimiza miezi sita ili kuwakinga na magonjwa ya kuhara.
Pia wanakijini walipata kuoneshwa filamu ya madhara ya pombe ambayo yanaweza kupelekea mtu kufanya maamuzi ambayo si sahihi na hivyo kumpelekea kujiweka katika hatari ya kupata maambukizi ya VVU.
Mbali na filamu hizo fupi pia wanakijiji walipata fursa ya kuangalia filamu ndefu kutoka nchini Irani inayoitwa I’m His Wife.
Vijijini ambavyo washapata warsha hiyo ni pamoja na Nungwi,Matemwe,Ndagaa and Ubago. Leo warsha hiyo itatolewa Bububu,ikiwafutiwa na Jumbi siku ya kesho na Bweleo siku ya Jumapili. Pia wanawake wa Chakechake watapata mafunzo hayo siku ya tarehe 7-8 mwezi huu.
MWISHO