Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) katika kuendelea kutoa ruzuku kwa taasisi za elimu kwa lengo la kuongeza ubora katika utoaji elimu, pamoja na miradi mingine imelenga kupanua wigo wa elimu jumuishi kwa ngazi mbalimbali za elimu nchini.
'Elimu jumuishi' ni ile inayotambua mahitaji tofauti ya kujifunza ya wanafunzi ili kuhakikisha wanawekewa mazingira bora yenye kukidhi mahitaji yao. Tanzania inatekeleza utaratibu huu baada ya kuridhiria mpango wa utekelezaji Elimu Maalum wa Salamanca mwaka 1994. Mpango unasisitiza kuwa watoto wote wajifunze kwa pamoja kadri inavyowezekana, bila kujali tofauti za kijiografia, maumbile, jinsia, uwezo wa kiakili. Changamoto ni kuhahakikisha kuna vifaa vya kutosha kukidhi mahitaji hayo.Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imesaidia kuongeza wigo wa utekelezaji wa mpango huu kwa kutoa vifaa mbalimbali vya kujifunzia na kufundishia wanafunzi wenye mahitaji maalum na vifaa saidizi. Jumla ya taasisi 119 tayari zimeshafaidika na wanafunzi 3,114 wamenufaika na vifaa hivyo.
Aidha misaada iliyotolewa ni pamoja na:-
(a) vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye ulemavu kama fimbo nyeupe, vifaa vya kuongeza usikizi, miwani mafuta maalum kwa wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi
(b) vifaa vya kujifunza na kufundishia kama mashine za maandishi ya nukta nundu, vifaa vya TEKNOHAMA kama kompyuta maalum kwa wasioona, mashine ya kutoa machapisho kwa nukta nundu, vitabu vya kiada vya lugha za alama.
(c) Ukarabati au ujenzi wa miundo mbinu kama madarasa, mabweni ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi wenye ulemavu;
(d) Kuboresha mazingira ya vyuo vya mafunzo ya walimu wa elimu maalum.