INGAWA Tanzania kuna makabila zaidi ya 120, kanga ni vazi linalotumiwa takribani na makabila yote na hasa katika shughuli za misiba, jambo linalodhihirisha kwamba ni sehemu ya utamaduni wa jumla kwa Watanzania.
Kanga ni vazi la kuheshimiwa kwa kuwa ni sehemu ya maisha ya Watanzania, wanawake wengi hutumia kanga kama vazi, wengine wanapenda kuzitumia kuwafunika watoto mara baada ya kuzaliwa, hutumika kutandika kitandani, pia hutumika kwenye ngoma za utamaduni na sherehe za ndoa.
Vazi hilo limewavutia watu wengi ikiwa ni pamoja na aliyekuwa mke wa balozi wa India nchini Adity Chakravarti ambaye ameamua kulienzi vazi hilo kwa kulitangaza ndani na nje ya nchi, “Ninaipenda sana Tanzania na nimeamua kuchora michoro mbalimbali yenye kuelezea mavazi na matumizi sahihi ya kanga ili niweze kuuenzi utamaduni wa Tanzania,” anasema Adity.
Adity anasema matumizi ya vazi la kanga ni sawa na vazi maarufu la sari nchini India kwa kuwa linagusa sehemu kubwa ya maisha ya Watanzania wote bila kujali kabila, dini wala kipato. Anafahamisha kuwa michoro yake inayoelezea juu ya mavazi na matumizi ya kanga ni zawadi kwa Watanzania kwa kuwa ana amini kuwa itadumu kwa muda mrefu na kutumiwa na watu mbalimbali kuelezea utamaduni na uzuri wa nchi ya Tanzania.
Amechora picha zinazoonesha wanawake wakiwa wamevaa kanga kwa mitindo mbalimbali kulingana na sehemu walipo na kwa kuzingatia utamaduni eneo husika.. Mfano picha zinazoonesha mandhari ya Zanzibar amechora wanawake waliojitanda ushungi kwa kutumia kanga wakati katika mandhari ya Morogoro amechora wanawake waliojifunga kanga kifuani.
Adity anasema alipata wazo la kutumia kipaji chake kuuenzi utamaduni wa Tanzania, mara alipotembelea mkoa wa Morogoro na kujionea jinsi wanawake wa vijijini wanavyopendeza wakiwa katika vazi la kanga. Baadhi ya wanawake wa Morogoro huvaa kanga kifuani na kuacha sehemu ya mabega yao wazi na kuendelea na kazi bila kanga kudondoka.
Wanawake hao wanatoa taswira ya Mwafrika halisi na vazi hilo linasaidia kuenzi utamaduni. Adity amechora picha zinazoonesha wanawake wa Morogoro wakiwa katika shughuli mbalimbali za maisha yao ya kila siku hasa kulima, kutwanga, kuvuna pia amechora picha zinazoonyesha baadhi ya wanawake wakiwa wamepumzika baada ya kufanya kazi nyingi.
Ili kutofautisha michoro za Morogoro na mikoa mingine, Adity amechora picha zinazoonesha mandhari ya Morogoro kama vile milima ya Uluguru, nyumba za msonge na shughuli za kiuchumi zinazofanywa katika mkoa huo kama vile kilimo cha ndizi.
Katika michoro yake, Adity ametumia rangi ya chungwa na kahawia kuelezea taswira alioona katika mkoa wa Morogoro, hususan uzuri wa rangi ya ngozi ya wanawake wa Kiafrika pia udongo wenye rutuba alioona katika mkoa wa Morogoro.
Pia anapenda kutumia rangi ya kijani kuelezea uzuri wa uoto wa asili nchini Tanzania ambao unamkumbusha umuhimu wa mboga za majani ambazo ni sehemu kuu ya chakula cha kila siku. Pia wanawake wa Zanzibar wavutia kwa jinsi wanavyotumia kanga kujifunika
kwa mujibu wa mila na desturi zanazozingatia kanuni za dini ya Kiislamu.
Hii inadhihirisha kwamba vazi la kanga linaweza kutumika kuimarisha imani ya kidini ambayo ni muhimu katika kujenga uhusiano na maadili mema katika jamii. Michoro ya Adity imechorwa kwa ustadi mkubwa na kwa mtindo wa kipekee kwa kuchoma baadhi ya vipande vya miti au mbao anazotumia kuchorea kisha kuviunganisha kwa makini, jambo linaloongeza mvuto kuangalia na kuzisoma picha hizo.
Anaeleza kuwa anapenda kutumkia mtindo wa kuchoma vipande vya mbao au mti anayotumia kuchora kama njia mojawapo ya kuhamasisha utunzaji wa mazingira. Anafafanua kuwa vipande vya mbao, miti, vitambaa au magunia vinaweza kutumika kama rasilimali inayotokana na taka rejea na kutumika kuzalisha bidhaa nyingine.
Alianza kutumia uchoraji wa kuchoma wakati alipokuwa akiishi Canada ambapo alikuwa akichukua vipande vya kuni zilizokuwa zinatumika kuoka moto wakati wa masika. Anapendelea kuchora kwenye mbao, vipande vya kitambaa au gunia pia huchora kwenye masanduku ya pembe nne yenye kimo tofauti ili watu wanaotaka masanduku wasikwazike kwa kusoka aina ya sanduku wanazotaka kulingana na matumizi yao.
Adity anawahimiza Watanzania kujikita katika sanaa ya uchoraji kwa kuwa ni njia mojawapo ya kuweka kumbukumbu ya kudumu kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Sanaa ya uchoraji inategemea ubunifu na bidii ya msanii husika kwa kuwa kila msanii anayependa kujiendeleza hupaswa kutumia ubunifu wa hali ya juu kuchora vitu bora zaidi bila kupoteza utambulisho wake ndio maana yeye ameamua kuendelea na ubunifu wa kuchoma michoro yake lakini anaendelea kutumia mbinu za kuifanya michoro yake itambulike kwa popote itakapoonekana.
Pamoja na kuwa na kipaji Adity amesomea fani ya sanaa ya uchoraji katika Chuo cha Sanaa cha South Delhi Polytechnic kilichopo New Delhi na baadaye katika chuo cha Xue Shi Qi kilichopo Beijing, China. Baada ya kuhitimu masomo alianza kazi ya kuchora picha mbalimbali kwa kutia nakshi kwenye mawe yanayopatikana baharini.
Pia huchora kwenye mbao na vitambaa na mwaka 1988 alifanikiwa kuandaa onyesho lake la kwanza lililofanyika Triveni Kala Sangam, New Delhi nchini India. Kuanzia wakati huo Adity amekuwa akiandaa maonesho ya kazi zake za sanaa ya uchoraji na wakati akiwa nchini aliandaa maonesho mbalimbali katika hoteli ya Golden Tulip.
Baada ya kuondoka nchini amekuwa akifanya maonesho yake sehemu mbalimbali duniani duniani kwa lengo la kuhamasisha sanaa ya uchoraji na kuishawishi jamii kupenda kununua bidhaa zinazotokana na sanaa kwa lengo la kuuenzi utamaduni na kudumisha mambo ya asili.
Baba yangu alipenda kuniambia kwamba bahati humfuata mtu aliyejiandaa kuipokea…nami napenda kutumia usemi huo kuwaasa wasanii wa Kitanzania ili wasichoke kujiandaa kupokea bahati iliyopo mbele yao…atakayejiandaa vyema ndiye atakayenufaika zaidi,” Adity anahimiza.
Anasema kazi za sanaa ya uchoraji hazijapata soko la uhakika kwa kuwa wananchi wengi hususan Tanzania hawajui thamani na umuhimu wa kuwa na michoro hiyo majumbani mwao lakini anaamini kwamba kadri siku zinavyosonga mbele ndivyo jamii inavyofunguka macho na kuenzi utamaduni wao.
Kinachotakiwa ni uhamasishaji…wasanii na wadau wa maendeleo ya utamaduni na sanaa wanatakiwa kutumia vyombo vya habari kutangaza umuhimu wa kazi za sanaa ya uchoraji,” Adity anaeleza. Pia wasanii wanatakiwa kutumia mbinu mbalimbali kujitangaza ikiwa ni pamoja na kuchora picha za bei nafuu na kuziweka kwenye masoko ya kawaida kama mkakati maalumu wa kutangaza soko.
Amewataka Watanzania waondokane na dhana potofu kuwa kazi za sanaa ni kwa ajili ya watalii au wageni pekee kwa kuwa kila jamii inatakiwa kuuendeleza na kuuenzi utamaduni wao wenyewe.