


……………………….
Na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza
Maofisa na Askari wa Jeshi la Magereza walioshiriki kikamilifu kwenye Maonesho ya Kibiashara ya 37(SASABA) Mwaka 2013 wamepongezwa na Uongozi wa Jeshi la Magereza kwa kufanikisha Ushindi wa Pili katika Maonesho ya Kibishara ya Mwaka huu.
Akizungumza na Washiriki hao kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, Dkt. Jumna Ally Malewa amesema kuwa Ushindi huo ni wa kujivunia kwa sababu mpambano ulikuwa mkubwa na Makampuni yaliyoshiriki mengi yana uzoefu mkubwa likiwemo Kampuni la Furniture Centre, Zanzibar Furniture, Maridadi Timber Works na Jeshi la kujenga Taifa.
“Nachukua fursa hii kuwapongeza kwa kazi nzuri mliyoifanya Mwaka huu, Ushindi huu wa nafasi ya pili umetokana na kupokea maelekezo yaliyokuwa yakitolewa mara kwa mara kutoka Ofisi ya Makao Makuu kwamba vifaa vya Maonesho viwe na unadhifu wa hali ya juu, Ubunifu mkubwa na umaliziaji bora”.
Aidha Kamishna Malewa amesisitiza kwamba pamoja na kazi hiyo nzuri waliyoifanya kwa Mwaka huu ya kuonesha Ubunifu hadi kufanikiwa nafasi ya Ushindi wa pili, nafasi hiyo iwe ni changamoto kubwa itumike kujipanga kwa Mwaka ujao wa 2014 ili Jeshi la Magereza liweze kurudi katika nafasi yake ya Kwanza.
Kwa upande wao Washiriki wa Maonesho ya Kibiashara ya Mwaka huu 2013 wameushukru Uongozi mzima wa Jeshi la Magereza ukiongozwa na Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja kwa kuwawezesha na kufanikisha ushiriki wao katika Maonesho ya Mwaka huu ikiwa ni pamoja na kupitisha Bajeti ya kutosha ya maandalizi hali iliyoleta hamasa kubwa kwa washiriki hao katika Maonesho hayo ya Kibiashara ya 37(SABASABA) Mwaka 2013.
Hata hivyo, Washiriki hao wameahidi kuendelea kufanya kazi zao kwa juhudi na maarifa ili kujenga na kulinda sifa ya Jeshi la Magereza na Nchi yetu kwa ujumla pamoja na changamoto mbalimbali zilizopo ambazo tayari Uongozi wa Jeshi la Magereza unaendelea kuzipatia ufumbuzi kadri inavyowezekana.