Na Lorietha Laurence
Kamati ya Bunge ya Kilimo,Mifugo na Maji imejadili pendekezo la Muswada wa Sheria ya Taifa ya Umwagiliaji ya mwaka 2013 ambao utatatua changamoto zinazokabili kilimo cha umwagiliaji pamoja na kuanzisha chombo cha kusimamia na kuratibu kilimo cha umwagiliaji nchini.
Sheria inayopendekezwa kutungwa itaanzisha Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ambayo itakuwa na chombo cha kusimamia sheria na kuainisha mamlaka na majukumu ya Waziri mwenye dhamana ya umwagiliaji kwa kuvutia sekta binafsi kushiriki kikamilifu na kuwekeza katika miundombinu ya umwagiliaji.
Muswada huo ulisomwa kwa mara ya kwanza Bungeni Juni 28, 2013 na unatarajiwa kusomwa tena kwa mara ya pili katika Bunge litakaloanza Agosti 27, 2013 mara baada ya kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali wa Kilimo.
Naye Waziri wa Kilimo,Chakula na Ushirika Bw.Christopher Chiza amesema mpango wa Serikali ni kufanya kilimo cha umwagiliaji kiweze kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuleta mapinduzi ya kijani na kuliwezesha Taifa kufikia lengo la kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 25 ifikapo mwaka 2015/2016.
“Nia ya kuwasilisha Muswada huu mbele ya kamati yako ni kupata maoni ya kamati na wadau wengine kabla ya Muswada haujawasilishwa Bungeni kwa kusomwa mara ya pili na hatimaye kupitishwa kuwa sheria kwa kuzingatia taratibu ”.alisema Bw.Chiza
Aliongeza kuwa ukuaji wa uchumi wetu lazima utegemee ukuaji wa kilimo kwa kushirikiana na sekta nyingine kama vile sekta ya afya kwa kuhakikisha wakulima wanakuwa na afya bora ili waweze kufanya shughuli za kilimo kwa ufanisi.
Pia mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye ni Mbunge wa Kilolo Bw.Peter Msola amesema asilimia 80 ya watanzania wanategemea kilimo hivyo kuna umuhimu wa kuboresha sekta ya kilimo cha umwagiliaji bila kutegemea mvua za msimu.