
Mlinzi mwenye silaha akilinda huko Ufukwe wa Lido mjini Mogadishu wakati watu wakisherehekea siku kuu ya Eid al-Fitr hapo tarehe 8 Agosti.
Vikundi vya asasi za kijamii vinatoa wito kwa serikali ya shirikisho na tawala za kanda kufanya maamuzi magumu juu ya usalama na sheria ili kuwashawishi Madaktari wasio na Mipaka (MSF) kubatilisha uamuzi wake wa kusitisha operesheni zake nchini Somalia.
Baada ya kuwahudumia Wasomali kwa zaidi ya miaka 22, shirika hilo la misaada la kimataifa liliamua kwamba hali ya usalama imekuwa mbaya sana kiasi ya kushindwa kuendelea na shughuli zake nchini.
Uamuzi huu umewaacha maelfu ya Wasomali bila ya huduma ya afya na wafanyakazi wa Somalia waliokuwa wanafanyakazi na MSF kuwa hawana ajira.
"Watu wa MSF wameuliwa na kutekwa, kwa hivyo serikali [ya shirikisho] na tawala za mikoa zinapaswa kuchukua dhamana ya usalama wa MSF na mashirika mengine ya misaada," alisema Abdullahi Mohamed Shirwa, mwenyekiti wa Watendaji Wasiokuwa wa Serikali wa Kusini na Kati ya Somalia (SOSCENSA).

Bendera iliyochanika ya Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) ikipepea juu ya zahanati iliyohamwa na kuendesha na shirika hilo hilo lisilo la kiserikali katika majengo ya Kambi za wakimbizi ya Dadaab nchini Kenya mwezi Oktoba mwaka 2011. [Na Tony Karumba/AFP]
Kwa kuzingatia ni kwa kiasi gani umma wa Somalia unategemea aina nyingi za misaada inayotolewa na nchi za kigeni na mashirika ya kimataifa, serikali inapaswa kufanya kazi bora zaidi ili kurahisisha kazi za wadau wa kimataifa, alisema Shirwa. "Serikali lazima iwalinde."
Dokta Lul Mohamed, mkurugenzi wa zahanati ya wajawazito na watoto katika Hospitali Kuu ya Benadir, alisema kuwa MSF walikuwa wamevunjwa moyo na mazingira ya wafanyakazi wake wanayofanyia kazi, ambayo yalikuwa hayaonekani kuwa bora zaidi.
"Ikiwa siku zote unafanyakazi katika mazingira magumu, na kila wakati unapofikiria mambo yatakuwa mazuri lakini badala yake yanakuwa mabaya zaidi, bila ya shaka hatimaye utashindwa," Mohamed aliiambia Sabahi.
Alisema kuwa mashirika mengine ya misaada yatafuata nyayo za MSF na kusitisha operesheni zao nchini ikiwa Somalia haitafanya mabadiliko ili kuhakikisha ulinzi wao.
"Serikali inapaswa kutunga mkakati wa wazi [kwa msaada wa matibabu] ili kuyahakikishia mashirika ya misaada au zijitosheleze na kufanyakazi ya kupata bajeti kwa ajili ya huduma za afya," alisema. "Kwa kweli MSF sio wa kulaumiwa."
Mbunge Mohamed Omar Dalha alisema kuwa MSF na wadau wengine wa kimataifa wamekuwa na wanaendelea kuwa watu wa lazima kwa ajili ya Somalia kujiweza upya.
"Msaada ambao mashirika haya yametoa kwa Wasomali kupitia kipindi kirefu cha kutokuwepo na utulivu na cha mgogoro wa kibinadamu umekuwa msaada mkubwa sana," alisema. "Wasomali wote wanapaswa sasa kuwajibika kulinda usalama wa waajiriwa wa mashirika ya misaada."
Akielezea kuondoka kwake wiki iliyopita, MSF ilisema, "makundi yenye silaha na viongozi wa kiraia wanaendelea kusaidia, kuvumilia au kufanyia mzaha mauaji, uvamizi na utekaji wa wafanyakazi wa msaada."
Waangalizi wengi siku za karibuni wameshauri kwamba serikali ya shirikisho ingetafuta msaada kutoka kwa vikosi vya kimataifa kutoa mafunzo na kuwapatia vifaa wafanyakazi wa usalama nchini kama njia ya kuimarisha hali ya usalama.
Serikali ya Somalia lazima iweke dhamana
La mwisho, ni kuwa serikali inachukua dhamana wa kuondoka kwa MSF, kwa mujibu wa mbunge Abdi Barre.
Alisema kuwa utawala ulishindwa kutoa viwango angalau vya chini vya usalama mjini Mogadishu, ambako kila mmoja anafikiria kuwa ndio kiwango cha kurejea kwa hali ya kawaida nchini Somalia.
Barre alisema serikali ilikuwa imepuuza kabisa kushughulikia kesi ya Ahmed Salad Farey ambae aliachiwa huru kutoka jela mwezi Januari 2013, kasoro ya mwaka mmoja baada ya kuwa alishahukumiwa miaka 30 jela kwa mauaji ya waajiriwa wa MSF, Dokta Karel Keiluhu na Phillipe Havet, mwaka 2011.
Wakati wa kuachiwa huru kwa Farey, vyombo vya habari vya ndani viliripoti mambo yasiyo ya kawaida yaliyofanywa na maafisa watatu wa mahakama kuhusiana na rufaa yake na hatimaye kuachiwa huru. "Baada ya kuhukumiwa alifungua rufaa na baadaye kuachiwa huru kwa kuharakisha," Jaji Mkuu Aydid Abdullahi Ilka-Hanaf alisema katika mkutano na vyombo vya habari hapo tarehe 8 Januari.
Ilka-Hanaf aliwaambia waandishi wa habari kuwa Farey aliondoka nchini baada ya kuachiwa huru lakini wapi alipo hasa hapajulikani. Pia alisema kuwa maafisa watatu waliohusika na kuachiwa kwake huru wameondolewa ofisini lakini hakuweka wazi iwapo watashitakiwa.
"Ikiwa muaji anatoroka, tungepaswa kuwachunguza wale waliomsaidia," Barre alisema, na kuongeza kwamba ikiwa serikali ingeishughulikia kesi ile vizuri zaidi watu wanaohudumiwa na MSF wasingekabiliwa na matokeo yake mabaya.
Raisi wa Kimataifa wa MSF Dk. Unni Karunakara alielezea wasiwasi wake juu ya uzembe uliotambulika katika kesi ile na maana gani inayoleta kuhusu hali ya usalama nchini Somalia.
"Mtu alikuwa amehukumiwa na mahaka ya Somalia, na kuhukumiwa kifungo cha miaka [30]," aliwaambia waandisi wa habari tarehe 14 Agosti. "Lakini miezi mitatu baadaye aliachiwa huru. Na hatujui yuko wapi, na hatuna habari kuhusu yukoje, anafanya nini, na kadhalika. Lakini sisi wasiwasi wetu ni kuwa hii inamaanisha ukosefu wa heshima, au aina ya kufumbia jicho mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa misaada na watu wanaotoa huduma kwa Wasomali."
Sababu ya kuondoka kwa MSF
Tukio, pamoja na al-Shabaab kuwateka wafanyakazi wawili wa Kihispania wa MSF kutoka katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab huko Kenya mwezi Oktoba 2011, lilisababisha MSF kupunguza shughuli zake huko Mogadishu kwa nusu na kufunga vituo vyake vikubwa viwili vya tiba jijini.
Chini ya mwezi mmoja baada ya wafanyakazi wa MSF kuachiwa huru, shirika hilo lilitangaza kuondoka kwake, kuashiria kwamba matukio haya yamekuwa sababu ya msingi ya MSF kuondoka Somalia.
"Matukio haya mawili ndiyo ya hivi karibuni katika mfululizo wa unyanyasaji mkali," MSF ilisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari tarehe 14 Agosti. "Wafanyakazi wengine kumi na nne wa MSF waliuawa na shirika hilo limekabiliwa na mashambulizi mengi kwa wafanyakazi wake, magari ya kubebea wagonjwa na huduma za tiba tangia mwaka 1991."
Saa chache baada ya shirika la kutoa misaada kutangaza kuwa linaondoka Somalia, wanamgambo wa al-Shabaab walipora hospitali ya MSF katika mikoa ya Bay na Jubba ya Kati.
Wakazi katika mikoa yote waliripoti kushambuliwa na wanamgambo wa al-Shabaab wenye silaha kali wakilazimisha kuingia kwenye hospitali na kuchukua vifaa vya matibabu, kompyuta na dawa.
Hii haikuwa mara ya kwanza kwa wanamgambo wa al-Shabaab kusababisha kutokuwa na usalama na kutumia nafasi hiyo ya kutawanyika kwa gharama ya ustawi wa watu wa Somalia.
Miongoni mwa ukame wa mwezi Julai 2012, al-Shabaab waliiba msaada wa kibinadamu wa chakula uliokusudiwa kutolewa kwa wananchi na badala yale kuutumia kuwalisha wapiganaji wake.
Al-Shabaab wamekuwa wakirudia kuyazuia mashirika ya kutoa misaada kufanya kazi katika maeneo ambayo wao wanayadhibiti, wakivuruga kampeni za chanjo ya kinga na misaada ya kawaida ya kimatibabu.
Wiki lililopita, Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza (DFID) ilikiri kwamba wanamgambo wa al-Shabaab waliiba msaada uliokuwa ukipelekwa Somalia wenye thamani ya Dola 750,000 kati ya mwezi Novemba 2011 na Februari 2012.
Waomba MSF kubadilisha uamuzi
Serikali ya shirikisho ya Somalia imeshangazwa na uamuzi wa MSF kusimamisha kazi zake za kibinadamu, alisema Ridwan Haji Abdiwali, msemaji wa waziri Mkuu wa Somalia Abdi Farah Shirdon. Alitoa wito kwa shirika hilo kufikiria tena uamuzi wake.
Abdiwali aliiambia Sabahi kwamba Wizara ya Kazi za Umma na Ujenzi Upya inatathmini kwa kina malalamiko yaliyoelezwa na MSF.
Hata hivyo, MSF walisema haikutosha kwa serikali ya shirikisho kuahidi kuboresha ulinzi, kwani usalama wa wafanyakazi wake hautegemei serikali pekee wakati wa mgogoro.
"Kazi yetu iko huru, ikimaanisha kwamba ulinzi wetu inabidi utokane na mapatano na wadau wote wanaohusika na jambo hili," alisema Ofisa Habari wa Kikanda wa MSF kwa Afrika Mashariki Heather Pagano.
Pagano alisema MSF inaweza kurejea katika shughuli zake nchini Somalia kama wadau wa kisiasa, wanamgambo na vyama vya kiraia watachukua hatua thabiti kuboresha hali hiyo.
"Inabidi waahidi kuheshimu kazi yetu na wafanyakazi ambao tunawaajiri kutoa huduma za matibabu kwa umma wa Somalia," aliiambia Sabahi.
Kujiondoa kwa MSF pia kumeathiri vituo vya matibabu katika mikoa ya Somaliland na Puntland.
Ahmed Omar Haji, gavana wa Togdheer, ambako MSF iliendeshea Hospitali ya Burao, alisema utawala wa mkoa wa Somaliland wakati wote husaidia na kuwalinda kishujaa wafanyakazi wa MSF .
"MSF haikukabiliwa na matatizo yoyote wakati ilipokuwa ikifanya kazi huko Somaliland," alisema, akitoa wito kwa shirika kuzingatia.
Waziri wa Afya wa Puntland Ali Abdullahi Warsame alisema, "MSF imekuwa na haraka kujitoa katika mikoa ya Puntland."
Warsame alisema MSF ilisimamia hospitali huko Bur Tinle na Galkayo, na kuondoka kwake kumeacha wagonjwa wengi wakiwahitaji, ikiwa ni pamoja na wale wanaopata matibabu ya kifua kikuu.
Mzee wa mila Nabaddon Mohamed Hassan aliiomba MSF kufikiria tena nafasi yake na kuvumilia hali ngumu ya usalama wa Somalia pamoja na Wasomali wasiokuwa na hatia na kuendelea kuusaidia umma, hususan katika Somalia ya Kusini ambako watu wanasumbuliwa chini ya utawala wa al-Shabaab.