
MSOMI na mchambuzi mahiri wa masuala ya siasa, Profesa Mwesiga Baregu
ameonya kuwa uamuzi wa baadhi ya vyama vya siasa nchini kuunda mabaraza
yao ya Katiba na kutoa mapendekezo ya Rasimu ya Katiba ni kuingilia
wawakilishi wa wananchi walioteuliwa kuunda mabaraza hayo.
Profesa Baregu ambaye ni mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alibainisha hayo jana wakati akifungua Baraza la Katiba la Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa akiwa Mwenyekiti wa kikao hicho cha siku tatu kilichoanza jana mjini Namanyere.
Alisisitiza, kuwa mabaraza ya Katiba ya wilaya yameundwa kwa ajili ya wananchi na si vinginevyo.
"Haya mabaraza ni rasmi na yameundwa kwa ajili ya wananchi ambapo yanatangulia kabla ya Bunge Maalumu la Katiba ... hapa wawakilishi wa wananchi mtatoa maoni yenu juu ya ugumu wa maisha, matakwa halisi ya
wananchi, huduma muhimu za nishati ya umeme, maji pia migogoro ya
wakulima na wafugaji," alisema Profesa Baregu, ambaye pia ni Mshauri wa
Alitaka wajumbe wa mabaraza ya Katiba ya wilaya nchini kutoa mapendekezo
ya wananchi waliowatuma na matakwa yao yanataka Katiba ya nchi hii iweje
miaka 200 ijayo ambao wengi wao wanaishi vijijini.
Pia alionya kama kazi ya kukusanya mapendekezo ya Rasimu ya Katiba
ikifanyika ovyo, baadaye wawakilishi wote watalaaniwa na umma.
"Wajukuu na vitukuu vyetu vitatuhukumu kwa kupiga viboko makaburi
tulimozikwa, lakini kama litafanyika kwa ufanisi, tutasifiwa na
halitaweza kurudiwa kwa zaidi ya karne mbili zijazo," alisisitiza. "Hizi
siku tutakazokaa na kutoa mapendekezo ya Rasimu ya Katiba ni muhimu
katika maisha ya Taifa letu," alisema Profesa Baregu.
Pia alionya kuwa Rasimu ya Katiba iliyopo si kiinimacho na mchezo wa
karata, huku akikanusha kuwa si kweli kuwa Tume iliyoandaa Rasimu
imepewa maagizo ya jinsi ya Katiba itakavyokuwa.
"Sio kiinimacho kilichomo humu ndani ya Rasimu hii, ni maoni ya watu
wote ... tumejitahidi kwa kadri ya uwezo wetu kuunganisha maoni ya
wananchi wote nchini ... isitoshe si mchezo wa karata, isitoshe si kweli
kuwa Tume imepewa maagizo ya jinsi ya kuandika hii rasimu," alisisitiza.
Profesa Baregu alilazimika kutoa ufafanuzi huo kutokana na hoja iliyotolewa katika mkutano huo wa Baraza la Katiba na Asante Edward aliyeonesha wasiwasi kuwa tayari Rasimu inayojadiliwa imeandaliwa tayari na kwamba wajumbe wa Baraza wanatekeleza wajibu tu.
Akiwatoa wasiwasi wajumbe, Profesa Baregu alisisitiza kuwa hata Rasimu ya pili itatokana na maoni ya Watanzania na si vinginevyo.
Chanzo: Habari Leo