RPC Mbeya Diwani Athuman
Na Esther Macha, Mbeya
WANAFUNZI kumi na tano(15) katika shule ya sekondari ya Wazazi ya Lupata Wilayani Rungwe Mkoani Mbeya wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa kosa la kuchoma moto bweni la shule hiyo kutokana na wanafunzi wenzao kusimamishwa masomo na uongozi wa shule kwa utovu wa nidhamu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ,Kamanda wa polisi Mkoani Mbeya Bw.Diwani Athuman alisema kuwa tukio lilitokea mei 14 mwaka huu majira ya saa 2.00 usiku katika shule ya sekondari Lupata.
Bw.Athuma alisema kuwa wanafunzi hao baada ya kuona wanafunzi wenzao watatu wamesimamishwa masomo walianza vurugu usiku na kuanza kuchoma moto bweni moja la wanafunzi wa kiume .
Aidha Kamanda Athuma aliwataja wanafunzi waliosimamishwa kwa utovu wa nidhamu shuleni hapo kuwa ni ,Joseph Robert (18) Kidato cha nne Mkazi wa Kitunda Jijini Dar es Salaam,Mwita Chacha(17),Mwanafunzi wa kidato cha tatu mkazi wa Jijini Dar es Salaam ,pamoja na Daniel David(18)kidato cha Tatu mkazi wa Ipinda Kyela.
“Hawa wanafunzi watatu waliosimamishwa masomo walihamasisha wenzao kuunga mkono kupinga adhabu hiyo kwa kufanya vurugu na kuchoma bweni hilo la wanafunzi”alisema Kamanda Athuman.
Alisema kuwa bweni lilochomwa moto walikuwa wanaishi wanafunzi ambao hawakuwa tayari kuunga mkono uvunjifu huo wa amani shuleni hapo.
Aidha Bw. Athuman alisema kuwa kufuatia vurugu hizo vinara wawili wa vurugu hizio wanashikiliwa na jeshi kwa mahojiano zaidi ambao ni ,Joseph Robert , Mwita Chacha huku watuhumiwa kumi na tano wanashikiliwa na jeshi hilo.
Kuhusu vitu ambavyo vimeharibiwa Kamanda huyo alisema thamani halisi ya uharibifu uliotokea bado kujulikana na kwamba hakuna madhara yeyote ya kibinadamu yaliyotokea .
Hata hivyo Bw.Athuman ametoa wito kwa jamii hasa wanafunzi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwani ni kinyume cha sheria na badala yake watatue matatizo kwa njia ya meza ya mazungumzo katika mamlaka husika ili kuepusha madhara na hasara zinazoweza kujitokeza ambazo mara nyingi wahanga wanakuwa ni wanafunzi wenyewe.
Mwisho.