
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka
Wizara ya Kazi na Ajira imetangaza kuongeza mishahara kwa sekta binafsi kwa kati ya asilimia 20 hadi 65, huku ikikusudia kuongeza nafasi za ajira zaidi ya 300,000 kwa mwaka 2013/14 na kujenga mazingira mazuri kwa ajira binafsi kupitia miradi mbalimbali.
Akitoa makadirio ya matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2013/14 jana, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka alisema wizara imekamilisha utafiti na majadiliano ya kima cha chini cha mshahara
katika sekta binafsi 12.
Sekta nyingine alizitaja kuwa ni Ulinzi Binafsi ( asilimia 46.4), Madini (asilimia 25.2), Afya (asilimia 65), Uvuvi na Huduma za Majini (asilimia 21.2), Usafirishaji (asilimia 49) na Kilimo (asilimia 46.4).
Kabaka alisema kuwa wakati wowote kuanzia sasa watatangaza viwango halisi vya mishahara kwa sekta hizo, baada ya kazi ya ukokotoaji kukamilika.
“Sekta nyingine mpya ambazo ni Ujenzi, Shule Binafsi, Nishati na Mawasiliano nazo zimepandishiwa viwango,” aliongeza Kabaka.
Katika hatua nyingine, Kabaka alisema katika kipindi cha mwaka 2013/14 serikali imekusudia kuzalisha zaidi ya ajira 100,000 ili kukabiliana na tatizo la ajira nchini.
Kabaka alieleza pia katika mwaka ujao wa fedha, serikali itatengeneza ajira 300,000 mbali ya nyingine 61,915 zitakazopatikana kwenye sekta ya Utumishi wa Umma.
Alisema pia kwa kupitia programu yake ya miaka mitatu, 2013/14 hadi 2015/16 itatengeneza ajira 600,000 kwa vijana.
“Serikali imelenga kujenga uwezo wa vijana wa kupata ujuzi na stadi mbalimbali za kazi,” alisema Kabaka.
Alizitaja stadi hizo kuwa ni kuwapatia mitaji na mikopo nafuu, kuwatengea maeneo ya uzalishaji na biashara, kuwalinda kisera na kisheria.
“Serikali kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na Benki ya CRDB itaandaa ajira kwa wahitimu wa elimu ya juu, ambapo miradi zaidi ya 200 ya kilimo na ufugaji itaanzishwa.
Alisema katika kipindi cha mwaka uliopita, Serikali imeweza kuandaa ajira 274,030.
Katika kipindi hicho, Kabaka alisema pia wameweza kutoa elimu kuhusu utambuzi wa haki na fursa za ajira kwa walemavu kwa waajiri 252 na vyama vitano vya walemavu.
Akizungumzia namna ya kufanikisha mfumo endelevu wa mkakati wa kuwapatia wazee wote nchini pensheni, Kabaka alisema Serikali inafanya utafiti na kuandaa mapendekezo.
Kuhusu kupambana na ajira kwa watoto, Kabaka alisema Serikali imejiandaa kuwaondoa watoto 8,000 wenye umri kati ya miaka mitano na 17.
Alisema alisema katika bajeti ya Sh2.1 bilioni alizotengewa katika mwaka wa fedha uliopita kwa ajili ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi, ni Sh1.5 bilioni tu walipatiwa sawa na asilimia 71.7.
Katika kipindi cha mwaka 2013/14, Kabaka alisema wizara yake inaliomba Bunge liidhinishe Sh15 bilioni kwa ajili ya mishahara na shughuli za maendeleo.
Hata hivyo, Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii iliishutumu Serikali kwa kutoipatia wizara hiyo fedha kulingana na wabunge walivyoiidhinishia katika mwaka unaoisha 2012/13.
“Hadi Machi (mwaka huu), fedha zilizotolewa ni Sh6.3 bilioni sawa na asilimia 48.3. Aidha wizara katika kipindi hicho haikupokea fedha kwa ajili ya maendeleo,” alisema Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Jenista Mhagama.
Alisisitiza kuwa hata kiwango kilichopangwa kwa mwaka ujao hakitoshi kulingana na majukumu mengi ya wizara hiyo.
Mhagama pia alizungumzia mifuko ya jamii, kuwa wizara inapaswa kusisitiza kuwepo na ruhusa ya fao la kujitoa.
Alisema wafanyakazi wengi hawana uhakika wa kufanya kazi kwa miaka 55 au 60 hivyo kuwaondolea fao la kujitoa ni sawa na kuwaangamiza kimaisha.
Mhagama alisema takwimu za mwaka 2002 zinaonyesha wastani wa umri wa Mtanzania kuishi ni miaka 47 hadi 53, hivyo, kuwanyima wafanyakazi fao la kujitoa ni kuwanyima haki za msingi.
Aliitaka serikali kuweka sheria inayoruhusu fao la kujitoa kwa wafanyakazi kutumia fao la kujitoa kwa ajili ya jambo lolote la msingi kwa maisha yake, kama vile kulipia mkopo wa nyumba.
Kambi ya Upinzani Bungeni ilielezea juu ya mifuko hiyo ya hifadhi ya jamii kuongozwa na watu wasio na uwezo.
Msemaji wa kambi rasmi ya upinzani kupitia wizara hiyo, Cecilia Paresso (Viti Maalumu - Chadema) alisema uongozi huo dhaifu ndiyo umekuwa ukichelewesha au kutoa mafao kidogo kwa wastaafu.
Paresso aliitaka Serikali iwapunguzie mzigo wa makato ya kodi ya Lipa kwa Kadri Upatavyo (PAYE), yapunguzwe na vilevile kiwango cha chini cha mshahara kukatwa kiwe ni Sh350,000.
Aliitaka Serikali kufafanua kuhusu Rais Jakaya Kikwete kutoa takwimu za mapato ya mifuko ya jamii ambazo zinatofautiana na zile za Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali (CAG).
Paresso alitoa mfano kwamba Rais Kikwete aliwahi kunukuliwa akisema kuwa mifuko hiyo inapata faida na kukua vizuri, wakati ripoti ya CAG alisema kuwa inapata hasara na ipo hatarini kufa.
Kambi ya upinzani ilipinga tabia ya Serikali kukopo kupitia mifuko hiyo na kutorejesha, kwamba kunachangia hatari ya kuiua mifuko hiyo
MWANANCHI