
Lewandowski

KLABU ya Chelsea imehamishia mawindo yake kwa mshambuliaji wa Borussia Dortmund, Robert Lewandowski katika harakati za kocha Jose Mourinho kusaka kiongozi wa safu ya ushambuliaji.
Mourinho hashawishiki na Fernando Torres na Demba Ba na wanataka mtu mwingine katika safu ya ushambuliaji kupambana na nyota kinda, Romelu Lukaku na mchezaji mpya aliyesajiliwa kwa Pauni Milioni 18, Andre Schurrle ambaye wazi atakuwa anacheza pembeni.
Lewandowski anataka kuachana na wana fainali hao wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, lakini Dortmund imegoma kumuuza kwa wababe wao, Bayern Munich, ambako alichagua.
Mwakilishi wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 amewasiliana na Chelsea, Manchester United, Real Madrid na Barcelona pamoja na Bayern juu ya uhamisho wa Pauni Milioni 25.
Dortmund haiko tayari kumuuza kwa Bayern, baada ya mabingwa hao wa Ujerumani na Ulaya kuwachukulia mchezaji wao mwingine, Mario Gotze kwa dau la Pauni Milioni 32 mwezi uliopita.
Wiki iliyopita, Mtendaji Mkuu wa klabu, Hans-Joachim Watzke aliliambia Bild: "Robert Lewandowski hatauzwa kwa FC Bayern mwaka 2013. Hiyo ni mwisho. Tumemuambia Robert na wakala wake sasa,"alisema.
Hiyo inaweza kufungua milango kwa Chelsea, ambao wanaendelea taratibu kuisaka saini ya thamani ya Pauni Milioni 54 ya mshambuliaji wa Napoli, Edinson Cavani.
Cavani anatakiwa kwa muda mrefu Chelsea, lakini Mourinho ni shabiki mkubwa wa Lewandowski aliyemshuhudia akifunga mabao manne dhidi ya timu yake ya zamani, Real katika Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu huu.
Chelsea bado pia inamfukuzia mshambuliaji wa Zenit St Petersburg, Hulk, lakini Manchester United haiko tayari kumruhusu Wayne Rooney ahamie Stamford Bridge. Chanzo: binzubeiry