
Na Maggid Mjengwa,
Ndugu zangu,
Simulizi za Mzee Madiba zinaendelea. Ikumbukwe, kuwa Mandela alifika Dar es Salaam kwa mara ya kwanza mwaka 1962. Na wakati huo Mandela hakuwa Rais wa ANC. Rais wa ANC aliitwa Oliver Tambo.
Akiwa Dar es Salaam, ilipangwa pia Mandela akutane na Bw. Oliver Tambo, Rais wa Chama chake aliyekuwa akiishi nje ya Afrika Kusini. Lakini, kwa vile Mandela alichelewa kwa wiki mbili kuianza safari yake kutokea Botswana , hivyo, Mandela aliachiwa ujumbe na Oliver Tambo, kuwa amfuate Lagos, Nigeria. Huko Oliver Tambo alikwenda kuhudhuria Mkutano wa Mataifa Huru ya Afrika.
Hivyo, Mandela akafunga safari kwenda Nigeria akitokea Dar es Salaam kupitia Accra, Ghana. Ndege aliyopanda ikatua kwanza Khartoum, Sudan. Hapo Mandela akakutana na msukosuko wa kwanza wa safari yake. Ni pale abiria walipopanga foleni kupita kwa watu wa forodha.
Mandela hakuwa na passport. Mfukoni alibeba nyaraka alizoandaliwa na Serikali ya Tanganyika kwa msaada wa Nyerere. Nyaraka hizo zilikuwa ni kama za kumtambulisha Mandela tu. Ziliandikwa
" This is Nelson Mandela, a citizen of the Republic of South Africa. He has permission to leave Tanganyika and return here." ( Nelson Mandela, Long Walk To Freedom)
Inatafsrika hivi; " Huyu ni Nelson Mandela, raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kusini. Ana ruhusa ya kuondoka Tanganyika na kurudi hapa".
Nyaraka hii iliandikwa kiufundi sana ili kumlinda Mandela. Tafsiri yake ni kuwa, kama Mandela angepatwa na matatizo njiani, basi, inazitaka mamlaka nyingine zifanye taratibu za kumrudisha Tanganyika , si Afrika Kusini anakosakwa na makaburu.
Hata hivyo, hata kwa wakati huo, nyaraka inaacha maswali kwa afisa yeyote wa uhamiaji. Mathalan, kama Mandela ni raia wa Afrika Kusini aliondokaje Afrika Kusini bila hati? Na kwa nini akimaliza safari yake asirudi Afrika Kusini bali Tanganyika? Hivyo, inatoa tafsiri pia kuwa, kiufundi, Mandela alifanywa kuwa ' Raia wa Muda wa Tanganyika!'.
Kwa hati hiyo , na kwa akili ya kawaida, mtu angetarajia Mandela aulizwe maswali kadhaa ya kuitolea ufafanuzi pale Uwanja wa Ndege wa Khartoum, Sudan. Ajabu ni pale Mandela alipomkabidhi hati ya kusafiria afisa wa Uhamiaji wa uwanja wa ndege wa Khartoum. Aliyekabidhiwa ni mzee wa makamo, afisa yule aliziangalia nyaraka za kusafiria za Mandela. Kisha akamtazama usoni Mandela, akamshika mkono, na akamwambia;
" My son, Welcome to the Sudan!"- Mzee yule afisa wa Uhamiaji alitamka akiwa na maana ya kusema; " Mwanangu, Karibu Sudan!" Kisha akagonga muhuri kwenye nyaraka zile za Mandela.
Tunaona, kuwa tangu wakati huo, Nelson Mandela alikubalika kama ' Mwana wa Afrika'. Na kuanzia hapo Khartoum, Mandela alizunguka katika nchi kadhaa za Afrika akiwa amebeba nyaraka hizo alizoandaliwa kutoka Tanganyika ya Julius Nyerere. Hakuna mahali aliposumbuliwa Mandela katika ardhi ya Afrika.
Lakini, kwenye ndege aliyopanda Mandela, miongoni mwa abiria alikuwamo Bw. Hymie Basner na mkewe. Hawa ni raia wazungu wa Afrika Kusini. Huyu bwana Basner alikuwa safarini kwenda Accra, Ghana. Basner na Mandela wanafahamiana tangu Afrika Kusini. Mandela aliwahi kuajiriwa kwenye kampuni ya Basner.
Mzungu huyu ni mwanaharakati wa siasa za mlengo wa kushoto. Naye alikuwa anatafutwa na Makaburu. Alikuwa safarini kwenda Ghana kuomba hifadhi ya kisiasa. Naye kama Mandela, hakuwa na passport. Alipofika Tanganyika akitokea Afrika ya Kusini, alisaidiwa nyaraka za kumwezesha kusafiri.
Mandela anasimulia; " Basner alikuwa nyuma yangu, naye alimkabidhi afisa yule wa Uhamiaji nyaraka kama za kwangu. Mzee yule afisa wa Uhamiaji aliziangalia kwa muda. Kisha akatamka kwa sauti ya kukaripia;
" What is this?"- Hii ni kitu gani?
" What is this piece of paper? It is not official!"
" Hiki kipande cha karatasi ni kitu gani? Hii si rasmi yenye kutambulika!" ( Nelson Mandela, Long Walk To Freedom, pg. 346)
Hapo Bwana Basner akajikuta matatani na watu wa Uhamiaji pale Uwanja wa Ndege wa Khartoum. Ni Nelson Mandela aliyekuja kumwokoa. Je, Mandela alitumia mbinu gani kumwokoa mwajiri wake wa zamani?
Hii ni simulizi endelevu...