
Na Maggid Mjengwa,
Ndugu zangu,
Kabla ya kuendelea na simulizi tupeane bashraf japo kwa uchache. Neno bashraf lina maana ya mrejesho.
Naam, ikumbukwe, kuwa Mandela alifika Dar es Salaam kwa mara ya kwanza mwaka 1962. Na wakati huo Mandela hakuwa Rais wa ANC. Rais wa ANC aliitwa Oliver Tambo.
Akitokea Dar es Salaam, Mandela Akafanya safari kwenda
Addis Ababa kupitia Accra, Ghana. Kwenye ndege aliyopanda Mandela, miongoni mwa abiria alikuwamo Bw. Hymie Basner na mkewe. Hawa ni raia wazungu wa Afrika Kusini. Huyu bwana Basner alikuwa safarini kwenda Accra, Ghana. Basner na Mandela wanafahamiana tangu Afrika Kusini. Mandela aliwahi kuajiriwa kwenye kampuni ya Basner.
Mzungu huyu ni mwanaharakati wa itikadi za mlengo wa kushoto. Naye alikuwa anatafutwa na Makaburu. Alikuwa safarini kwenda Ghana kuomba hifadhi ya kisiasa. Naye kama Mandela, hakuwa na passport. Alipofika Tanganyika akitokea Afrika ya Kusini, alisaidiwa nyaraka za kumwezesha kusafiri.
Mandela anasimulia; " Basner alikuwa nyuma yangu, naye alimkabidhi afisa yule wa Uhamiaji nyaraka kama za kwangu. Mzee yule afisa wa Uhamiaji aliziangalia kwa muda. Kisha akatamka kwa sauti ya kukaripia;
" What is this?"- Hii ni kitu gani?
" What is this piece of paper? It is not official!"
" Hiki kipande cha karatasi ni kitu gani? Hii si rasmi yenye kutambulika!" ( Nelson Mandela, Long Walk To Freedom, pg. 346)
Hapo Bwana Basner akajikuta matatani na watu wa Uhamiaji. Ni pale Uwanja wa Ndege wa Khartoum. Ni Nelson Mandela aliyekuja kumwokoa. Je, Mandela alitumia mbinu gani kumwokoa mwajiri wake wa zamani?
Basner alijaribu kueleza kwa utulivu namna alivyopewa nyaraka hizo za kusafiria kutoka nchi ya Tanganyika. Kwamba ni kweli yeye hakuwa na passport.
" Not have a passport!"
Afisa yule wa Uhamiaji alimwuliza Basner kwa sauti na kuonyesha kumshangaa.
" Kwa nini usiwe na passport wakati wewe ni Mzungu?!" Aliuliza afisa yule wa Uhamiaji kwa kushangaa.
Basner akajibu kuwa amekimbia mashtaka nchini kwake kwa vile amekuwa akipigania haki za weusi.
Afisa yule Msudan akazidi kuonyesha mashaka na mshangao;
" Lakini wewe ni Mzungu!"
Mandela anasimulia, kuwa mwenzake mwingine safarini, Joe Mathews, alimwangalia Mandela na akajua anachofikiri Mandela. Joe akamnong'oneza Mandela, kuwa asiingile kwenye sakata lile kwa vile wao; Mandela na Joe ni wageni wa Serikali ya Sudan na wasije wakavuruga ukarimu wao waliouonyesha kwao.
Lakini, Mandela akafikiri, kuwa pamoja na kuwa Basner alikuwa ni mwajiri wake wa zamani, bado Basner alikuwa ni miongoni mwa weupe wachache waliojitoa muhanga kutetea ukombozi wa mtu mweusi. Hivyo, asingeweza kumsaliti katika hali ile.
Kimsingi Mandela angeweza kujiendea zake akiwa na mwenzake Joe, lakini, Mandela akaamua kubaki hapo hapo na kufuatilia sakata lile kwa karibu.
Na Mandela anasimulia, kuwa kila wakati Basner alipokuwa akimfafanulia jambo afisa yule wa uhamiaji wa Kisudan, yeye Mandela alikuwa aliinamisha kichwa taratibu mbele ya afisa yule wa uhamiaji kuashiria kuthibitisha ufafanuzi huo wa Bwana Basner.
Mzee yule afisa wa uhamiaji akatambua haraka lugha ya ishara kutoka kwa Mandela, naye akaanza kulainika. Akagonga muhuri wa uhamiaji kwenye nyaraka zile kutoka Tanganyika. Kisha afisa yule wa Uhamiaji akatamka;
" Welcome to the Sudan!"
Naam, tunaona hapa, kuwa Mzee Mandela aliianza kazi ya usuluhishi na upatinishi tangu enzi hizo angali kijana. Na kwenye tukio hili la Uwanja wa Ndege wa Khartoum, Sudan, tunaona jinsi Mandela anavyojipambanua na kuifanya kazi hiyo bila hata kutumia maneno.
Na ilikuwaje basi pale Mandela alipofika Ethiopia, nchi ya Mfalme Haile Selassie?
Hii ni simulizi endelevu...
0754 678 252
PS: Kumbukumbu muhimu:
Nelson Nolihlahla Mandela, miaka 95.
Miaka 67 ametumikia jamii.
Miaka 5 ametumikia nchi kama Rais madarakani.
Miaka 27 amekaa jela akiwa mfungwa namba '46664'.
Mandela amekufa, lakini, kwenye mioyo ya walimwengu ataendelea kuishi daima milele.