
Na Maggid Mjengwa,
Ndugu zangu,
Kwenye safari yake ya kwenda Ethiopia tumeona, kuwa Nelson Mandela alitua kwanza Kharthoum. Basi, akiwa pale Sudan, baadae akaelekea Ghana. Kule Ghana Mandela alikutana na Oliver Tambo, kiongozi wa ANC aliyekuwa akiishi na kufanya kazi za ANC akiwa mafichoni. Nje ya Afrika Kusini.
Mandela alikuwa hajaonana na Oliver Tambo yapata miaka miwili. Alishangaa kumwona Oliver Tambo amebadilika, si yule aliyekuwa akitokea katika staili ya mavazi ya kihafidhina. Oliver Tambo akawa ni mtu aliyefuga madevu na staili ya mavazi iliyobadilika. Alionekana mpiganaji zaidi.
Na hatimaye Mandela akafika Addis Ababa, Ethiopia. Akiwa Ethiopia, na kwa kupitia maandiko kwenye kitabu chake ' Long Walk To Freedom', Mandela anasimulia; kuwa ilikuwa ni mara yake ya kwanza kukutana na Mfalme aliyeongoza dola yake katika Afrika. Ni Mfalme Haile Selassie. Mandela alishangaa sana kumwona Mfalme mwembamba kwa maumbile lakini mwenye kuonyesha kuwa ni mwenye mamlaka makubwa.
Siku ya pili yake tu, Mandela aliuhudhuria gwaride la kijeshi ambapo Mfalme Haile Selassie alikuwa mgeni rasmi. Mandela ikawa mara yake ya kwanza kuona gwaride la wanajeshi mia tano Waafrika weusi likiongozwa na makamanda weusi. Jambo hilo lilimfurahisha na kumtia nguvu Mandela.
Mandela anaielezea zaidi Ethiopia, nchi ambayo zamani ikiitwa Abyssinia. Kuwa ni dola iliyokuwapo kabla ya kuzaliwa Kristo. Inasemwa, kuwa Ethiopia ni himaya iliyoasisiwa na mwana wa Mfalme Suleiman na Malkia wa Sheba.
Hata kama Ethiopia imepata kuvamiwa mara zaidi ya 12, lakini, Ethiopia inabaki kuwa ni chimbuko la harakati za kupigania utaifa kwa bara la Afrika. Ethiopia ndio dola ya Kiafrika iliyoanza kupambana na ukoloni, na si mara moja. Mfalme Menelik alipambana na kuwashinda wavamizi wa Kiitalia karne iliyopita.
Na mwaka 1930 Mfalme Haile Selassie akatwaa mamlaka ya himaya ya Ethiopia. Mandela anakumbuka alikuwa na umri wa miaka 17 tu, pale Fashist Mussolini wa Italia alipoivamia Ethiopia. Ni uvamizi uliomfanya Mandela sio tu azidi kumchukia Mussolini, bali kuuchukia ufashisti kwa ujumla wake.
Mfalme Haille Selassie akalazimika kuikimbia Ethiopia kufuatia uvamizi ule wa mwaka 1936. Hata hivyo, Mfalme Haile Selassie alirudi tena madarakani baada ya vikosi vya washirika kuwaondoa Waitalia nje ya Ethiopia mwaka 1941.
Mandela anasema; kuwa Ethiopia siku zote imekuwa na nafasi maalumu katika hisia zake. Kuitembelea Ethiopia ni sawa na kuchimbua mizizi ya historia na kufahamu chimbuko la Uafrika wake. Na kwa Mandela, anaamini, kuwa safari ya kwenda Ethiopia ilimvutia zaidi kuliko ukichanganya safari za kwenda Ufaransa, Uingereza na Marekani kwa pamoja. Na akawaza, kuwa kukutana na Mfalme Haile Selassie, ' Simba wa Yudah' ingekuwa jambo kubwa sana. Ni sawa na kushikana mikono na historia.
Kwa Mandela, Addis Ababa pamoja na kuwa ni Makao Makuu ya Mfalme, haikuonekana kuwa ni mji mkubwa na wa kisasa. Ilikuwa na mitaa michache, na hata mbuzi walionekana wakirandaranda mitaani. Mandela anasimulia; kuwa Addis Ababa kulikuwa na mbuzi zaidi kuliko magari barabarani. Ilikuwa ni tofauti kubwa na jiji la Johannesburg.
Ethiopia haikuonekana pia kuwa mfano katika demokrasia. Hakukuwa na vyama vya siasa wala mgawanyo wa madaraka. Ni Mfalme tu aliyekuwa kila kitu.
Wakiwa Ethiopia, ikafika wakati wa Mandela na Oliver Tambo kuhudhuria mkutano wa viongozi wa Afrika, ambapo, maombi ya ANC ya kutambuliwa rasmi yangejadiliwa pia.
Mandela na Tambo wakashangazwa kugundua, kuwa maombi yao yameshakwamishwa. Ni mjumbe kutoka Uganda aliyeyakwamisha akidai kuwa ANC ni chama cha kikabila.
Ni hapa, Mandela anakutana na changamoto inayomlazimisha, mbele ya viongozi wa Kiafrika, ajenge hoja zenye mashiko za kuifanya ANC iliyochafuliwa na PAC isafishike na ikubalike. PAC walikipakazia kwa viongozi wa Kiafrika, kuwa Chama Cha ANC ni chama cha kikabila. Ni hapa pia, Mandela kijana alipoanza kuonyesha uwezo na karama alizo nazo katika uongozi.
Je, Mandela aliyekuwa mtu wa pili kuongea baada ya hotuba ya ufunguzi ya Mfalme Haile Selassie alipambana vipi kuitetea ANC, mbele ya ' Simba wa Yudah!?
Hii ni simulizi endelevu...